#Athletics #Sports

BINGWA WA ZAMANI WA U20 KUONJA BERLIN HALF MARATHON

Chipukizi wa Kenya Benson Kiplangat imeratibiwa kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya half Marathon jijini Berlin Jumapili hii, ikiondokea mbio za masafa mafupi kuingia masafa marefu.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 22, alitangaza uwepo wake katika fani ya riada katika mbio za ubingwa wa wanariadha wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka wa 2021, ambako aliibuka mshindi wa mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 13:20.37.

Licha ya bingwa huyo wa zamani kuwa limbukeni katika mbio za barabara, ataingia jiji la Berlin akiwa tayari ameonyesha kasi ya aina yake kwenye mbio hizo, ikiwemo mbio za kilomita 10 katika eneo la Ibiza nchini Uhispania ambako aliwaongoza wakenya wenza kunyakua nafasi zote 3 za kwanza jukwaani.

Atashiriki mashindano ya Jumapili baada ya msimu wenye majaribu wa mwaka wa 2025, ambako alifungua mwaka kwa kumaliza wa 7 katika mashindano ya Shanghai Diamond League kwenye mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 13:09.90, akimaliza nyuma ya Berihu Aregawi, Kuma Girma na Mezgebu Sime wa Ethiopia waliomaliza chini ya dakika 13.

Hata hivyo, Kiplangat anatarajiwa kukumbana na ushindani mkali, atakapomenyana uso kwa uso na Bereket Nega wa Ethiopia, ambaye ni bingwa mtetezi wa Royadh Half Marathon, na kuhakikisha kuwa mkenya huyo anaingia moja kwa moja kwenye ubatizo wa moto.

Katika mbio za wanawake, Mkenya Veronica Loleo atalenga kuendeleza rekodi yake ya kuridhisha.

Amewahi kushinda mbio la Lilac Bloomsday 12K, Boilermarker 15K, na Buenos Aires Half Marathon, kabla ya kumaliza wa tatu katika mashindano ya Valencia Half Marathon nyuma ya Agnes Ng’etich na Fotyen Tesfay.

Atakutana uso kwa uso na Likina Amebaw wa Ethiopia, ambaye ni mshikilizi wa ubingwa wa Copenhagen Half Marathon, anayewasili katika mbio hizo akipumua moto baada ya kumaliza wa pili katika mbio za Valencia 10K.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *