AFCON 2025: CAS YATHIBITISHA KUPOKEA RUFAA YA SENEGAL
Mahakama ya usuluhishaji wa migogoro ya michezo, CAS, imethibitisha kupokea rufaa kutoka kwa timu ya taifa ya Senegal inayolenga kubatilisha uamuzi wa kupokonya ubingwa wa AFCON 2025.
Shirikisho la soka barani Afrika, CAF, lilitangaza uamuzi huo tarehe 17 mwezi huu wa kuwapokonya Senegal ubingwa na kuwavika Morocco, miezi 2 baada ya kukamilika kwa fainali iliyokumbwa na utata wa wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani na kisha kurejea tena.
Hatua hiyo ilisababisha Senegal kupokonywa ubingwa licha ya kushinda mechi ya fainali kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco, CAF ikisema hatua hiyo ilikuwa sawa na wao kukosa kufika uwanjani kwa mechi.
Wenyeji wa mashindano hayo Morocco, walipewa ushindi wa mabao 3-0 kwa mujibu wa kanuni za AFCON, na kutamatisha kiu chao cha miaka 49 cha kusubiri taji la pili la ubingwa wa mashindano hayo.
Hata hivyo, kupitia taarifa, CAS imesema kuwa itabuni jopokazi la kushughulikia rufaa ya Senegal.
Mkurugenzi mkuu wa CAS Matthieu Reeb, amesema mahakama hiyo ina uwezo wa kutatua mzozo huo, kwa usaidizi wa wataalam na wapatanishi huru.
Senegal ina siku 20 kuwasilisha hoja zake za kisheria.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 







































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































