SALAH KUIAGA LIVERPOOL MWISHONI MWA MSIMU
Mshambulizi wa klabu ya Liverpool Mohammed Salah, ametangaza kwamba ataondoka kwenye klabu hiyo ya Uingereza mwishoni mwa msimu huu, huku akiishukuru kwa kumpa alichokitaja kuwa wakati mwafaka zaidi wa maisha yake.
Liverpool imesema tayari wamekubaliana kuachana na Salah ambaye amewajibikia klabu hiyo kwa miaka 9, na ataondoka kama mchezaji huru.
Mkataba wake aliotia saini Aprili mwaka jana, utakatizwa kabla ya kukamilika kwa mwaka mmoja kufuatia msimu mgumu kwa fowadi huyo mwenye umri wa miaka 33 ikilinganishwa na misimu ya awali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Liverpool, Salah alichukua uamuzi wa kutoa tangazo hilo mapema kwa mashabiki ili kuweka wazi mustakabali wake kutokana na heshima na shukrani aliyo nayo kwao.
Raia huyo wa Misri, ambaye ni moja kati ya wachezaji mahiri katika historia ya Liverpool, atawaaga mashabiki wa Liverpool ugani Anfield kwenye mechi ya mwisho ya msimu itakayokuwa dhidi ya Brentford tarehe 24 mwezi Mei.
Salah aliwasili Anfield kutoka AS Roma ya Italia kwa kima cha pauni milioni 34 Julai mwaka wa 2017, na ndiye mchezaji wa 3 katika kuifungia Liverpool mabao mengi zaidi, na ataondoka akiwa ameshinda ligi kuu ya EPL, ligi ya mabingwa bara Ulaya, FA na Carabao Cup.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































