MBAPPE KIKOSINI, BELLINGHAM NJE DHIDI YA CITY
Mshambulizi wa Real Madrid Kyllian Mbappe amejumuishwa kwenye kikosi cha klabu hiyo kitakachomenyana na Manchester City leo usiku kwenye mechi ya mkondo wa pili ya raundi ya 16 ya ligi ya klabu bingwa bara Ulaya.
Mbappe mwenye umri wa miaka 27 ambaye alikosa mkondo wa kwanza kutokana na jeraha la goti, anatarajiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya City, Real tayari wakiwa mbele kwa mabao 3-0 kutokana na ushindi kwenye mkondo wa kwanza.
Mabao yote yalifungwa na kiungo Federico Valverde, na kuwapa vijana wa Pep Guardiola deni kubwa, na sasa watahitaji kupata ushindi wa zaidi ya mabao 3 ili kufuzu robo fainali.
Akizungumza na wanahabari hapo jana, kocha mkuu wa Real Alvaro Arbeloa, alithibitisha kwamba kiungo Jude Bellingham hatacheza licha ya kusafiri, akisema bado hajapona vizuri.
Katika mechi nyingine za usiku wa leo, Sporting watakuwa nyumbani dhidi ya Bodo/Glimt, Sporting wakiwa na mzigo sawa na Man City wa magoli matatu.
Chelsea waliodhalilishwa kwa kichapo cha mabao 5-2 na bingwa mtetezi PSG, watalenga kubatilisha matokeo hayo, wakihitaji pia kushinda na zaidi ya mabao 3.
Baada ya kupigwa breki kwa mara ya kwanza katika dimba hilo msimu huu walipoandikisha sare ya bao 1-1, Arsenal watakuwa wenyeji wa Bayer Leverkusen, ushindi wa aina yoyote kwa moja kati ya timu hizo ukiiwezesha kuingia robo fainali mwezi ujao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































