UCL: LIVERPOOL, BARCA WABANDULIWA, ARSENAL WAKIJIANDAA
Ousmane Dembele alifunga mara mbili na kuikabidhi timu yake ya Paris St-Germain ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool na tiketi ya kufuzu kwa awamu ya nusu fainali ya dimba la klabu bingwa bara Ulaya.
Ushindi huo uliipa Liverpool kichapo cha jumla ya mabao 4 bila jibu, na kuwabandua nje ya mashindano hayo katika awamu ya robo fainali, mbali na kuhakikisha kuwa vijana hao wa Arne Slot wanamaliza msimu bila taji lolote.
Liverpool walitamalaki kipindi kirefu cha mchezo ila wakashindwa kubuni nafasi za ufungaji, kabla ya Ousmane kujitokeza katika dakika ya 72 na kuwazika kabisa.
Aligonga msumari wa mwisho kwenye jeneza la the Reds katika dakika za majeruhi, na kuwaweka mabingwa hao watetezi PSG katika nafasi ya kulinda taji lao.
PSG watakutana na mshindi kati ya Real Madrid na Bayern Munich.
Katika matokeo mengine, Atletico Madrid waliponea mashambulizi ya Barcelona kufuzu katika awamu ya nusu fainali ya kombe hilo, licha ya kupoteza nyumbani kwa mabao 2-1.
Vijana wa Diego Simeone walianza mechi ya jana wakiwa kifua mbele kwa mabao 2-0 kutokana na ushindi wa mkondo wa kwanza, na walijipata chini ya shinikizo, Lamine Yamal akiwafungia Barca bao baada ya dakika 5 pekee za mchezo.
Dakika 19 baadaye, timu hizo zilikuwa na sare ya mabao 2 baada ya Ferran Tores kutia wavuni pasi ya Dani Olmo, na kuwazima kwa muda mashabiki wa nyumbani.
Hata hivyo, Ademola Lookman aliwanyanyua tena baada ya kumegewa pasi na Marcos Llorente katika dakika ya 31, Atletico wakilazimika kulinda uongozi wao hadi mwishoni mwa mchezo na kumaliza kwa jumla ya mabao 3-2.
Ilivyofanyika katika mkondo wa kwanza, Barcelona walionyeshwa tena kadi nyekundu, mwathiriwa wa jana akiwa Eric Garcia aliyemtega mshambulizi wa Atletico Alexander Sorloth.
Mechi za mwisho za mkondo wa pili zitapigwa leo.
Arsenal walio na uongozi wa bao 1-0 wataialika Sporting CP, huku Real Madrid wakielekea Munich kumenyana na Bayern, wanaoongoza kwa mabao 2-1.
Mshindi kati ya Arsenal na Sporting atakutana na Atletico Madrid huku Bayern ama Real wakimenyana na PSG katika semi fainali.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 






































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































