#Football #Sports

FIFA SERIES: STARLETS WAKALIFISHWA NYUMBANI NA AUSTRALIA

Timu ya taifa ya soka ya wanawake Harambee Starlets itahitajika kufanya mabadiliko ya kimfumo ili kuondoa udhaifu uliowekwa wazi kwenye kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Australia kwenye fainali ya FIFA Series hapo jana.

Mabao hayo yalitokana na makosa kadhaa katika safu ya ulinzi, mwanzo, Sam Kerr akiwaweka The Matildas kifua mbele baada ya safu ya ulinzi ya Kenya kushindwa kuondoa mpira wa kona, mpira huo ukiteleza mikononi mwa mlinda lango Lilian Awour na kuingia wavuni.

Kipindi kilichofuata kilishuhudia Kenya ikipoteza nafasi kadhaa za wazi, huku Awour akiwa na wakati mgumu kudaka mipira kutokana na mashambulizi ya Australia wanaoorodheshwa katika nafasi ya 15 duniani.

Fasila Odhiambo alishindwa kusawazisha akiwa kwenye kijisanduku na badala yake mpira ukatoka nje huku kombora lake Shaylene Opisa likipanguliwa na kipa wa Australia.

Wing’a wa Everton Clare Wheeler aliifungia Australia la pili kunako dakika ya 55, baada ya kuwapita mabeki kadhaa wa Starlets kuihakikishia timu yake ubingwa wa mashindano hayo ya kirafiki ya FIFA Series.

Kenya ilitinga fainali hiyo baada ya kuwalaza India kwenye mechi ya ufunguzi Jumamosi, nao the Matildas wakifuzu baada ya kuwabandua Malawi.

Kibarua sasa ni kwa kocha Beldine Odemba, kufanyia kazi mapungufu ya kikosi chake kinachojiandaa kwa mashindano ya WAFCON 2026.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *