SERIKALI YASITISHA MKATABA WA BARABARA NA KAMPUNI YA KIFARANSA
Serikali ya Kenya imesitisha mkataba wa euro bilioni 1.3, sawa na takriban shilingi bilioni 190.8, uliokuwa umeafikiwa na muungano wa kampuni kutoka Ufaransa ukiongozwa na Vinci SA, kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya kilomita 140 kutoka Nairobi hadi Nakuru.
Mkataba huo ulisainiwa mwaka 2020 jijini Paris wakati wa ziara ya rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta, barabara hiyo ikilenga kubadilishwa kutoka njia moja hadi ya njia nyingi kupitia mpango wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
KeNHA imesema masharti ya mkataba huo yangeiwekea serikali mzigo wa kifedha endapo idadi ya magari itakayoitumia barabara hiyo itakuwa ndogo na hivyo kutoa notisi ya kusitisha mkataba huo.
Kwa sasa, dur zinaeleza kuwa serikali inapanga kumpa mkandarasi kutoka China kazi hiyo, ingawa jina halijatangazwa rasmi. Waziri wa Fedha John Mbadi tayari ameongoza ujumbe wa mazungumzo Beijing, na Rais William Ruto anatarajiwa kuzuru China mwishoni mwa mwezi huu.
Imetayarishwa na Mercy Asami
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































