ARTETA AHOFIA MAJERAHA TISHIO KWA ARSENAL
Meneja wa Arsenal Mikel Arteta, amehofia kuwamba ongezeko la matatizo ya majeraha litatatiza azma ya klabu hiyo kutwaa taji la ligi kuu ya Uingereza EPL msimu huu, baada ya kiungo Declan Rice na beki wa kati Cristhian Mosquera kuondoka uwanjani wakichechemea jana usiku.
Wawili hao walikuwa nguzo kwenye ushindi wa Arsenal wa mabao 2-0 dhidi ya Brentford kutokana na magoli ya Mikel Merino na Bukayo Saka, na kurejesha pengo la pointi 5 kati yao na Manchester City walio katika nafasi ya 2.
Aidha, ushindi huo uliongeza msururu wa mechi 18 bila kupoteza katika mashindano yote kwa The Gunners, na ushindi wa 8 mfululizo nyumbani.
Hata hivyo, Arteta ambaye tayari anakosa huduma za mabeki wa kati Gabriel Magalhaes na William Saliba kutokana na majeraha, amepata pigo jingine la majeraha kwa Rice na Mosquera.
Arteta ambaye pia anakosa huduma za washambulizi Kai Havertz na Leandro Trossard, alilazimika kuwaleta mchezoni Saka, Jurrien Timber na Eberechi Eze aliokuwa ameamua kuwapumzisha wanapojiandaa kumenyana na Aston Villa Jumamosi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































