DIALLO ANG’AA KWA IVORY COAST
Kiungo wa Manchester United Amad Diallo alikuwa nyota mchezoni jana usiku wakati mabingwa watetezi wa dimba la taifa bingwa barani Afrika AFCON 2025 Ivory Coast waliwadhalilisha Burkina Faso kwa kibano cha mabao 3-0 kwenye awamu ya mwondoano, Ivory Coast wakiwa mabingwa watetezi wa kwanza wa AFCON kufika awamu ya robo fainali tangu mwaka wa 2010.
Diallo alifunga bao la ufunguzi na kutoa asisti ya bao la Yan Diomande kabla ya kutamatika kwa kipindi cha kwanza, nguvu mpya Bazoumana Toure akikamilisha ufungaji katika jimbo la Marrakesh nchini Morocco.
Ivory Coast sasa watafunga safari ya kuelekea kwenye mwambao wa pwani ya Morocco katika jiji la Agadir kumenyana na mshikilizi wa rekodi ya ubingwa wa AFCON Misri katika awamu ya robo fainali Jumamosi usiku.
Wakati uo huo, Algeria yake Riyad Mahrez ilijikatia tiketi ya robo fainali baada ya kuwanyuga DR Congo bao 1-0, na sasa watapambana na Nigeria katika mechi inayotarajia kuonyesha fataki kutokana na uwezo wa timu zote kushambulia.
Mechi nyingine za robo fainali ni Mali dhidi ya Senegal, na Morocco dhidi ya Cameroon.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































