MAREKANI YASITISHA UFADHILI WA USALAMA WA UN KWA HAITI
Marekani imesitisha mchango wake wa dola milioni 13.3 kwa mfuko wa umoja wa mataifa UN unaofadhili kikosi cha usaidizi wa usalama nchini Haiti, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Rais Donald Trump kupunguza msaada wa nje.
Baraza la Usalama la UN liliidhinisha kikosi hicho mnamo Oktoba 2023 kusaidia Haiti kupambana na magenge ya uhalifu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ameonya kuwa kuchelewesha msaada kunaweza kusababisha taasisi za usalama za Haiti kuporomoka na magenge kuteka mji mkuu, Port-au-Prince.
Marekani ilikuwa tayari imetoa dola milioni 15 kwa mfuko wa UN, mchango wa pili kwa ukubwa baada ya dola milioni 63 za Canada. Hapo awali, chini ya Rais Joe Biden, Marekani ilitoa zaidi ya dola milioni 300 kwa MSS, ikiwemo magari ya kivita.
Haiti kwa sasa haina rais wala bunge na inaongozwa na serikali ya mpito inayokabiliana na machafuko makubwa. UN inaripoti kuwa zaidi ya watu 5,626 waliuawa mwaka jana kutokana na ghasia za magenge, huku zaidi ya milioni moja wakiyakimbia makazi yao.
Imetayarishwa na Janice Marete
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































