ARSENAL WAKANYAGA GANDA LA NDIZI ETIHAD, CHELSEA WATAPATAPA
Manchester City iliikaribia ubingwa wa taji la ligi kuu ya soka nchini Uingereza kutokana na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani Etihad dhidi ya Arsenal katika pambano lililotajwa kama la kuamua ni wapi taji hilo litaelekea msimu huu.
Mshambulizi Erling Haaland aliihakikishia City ushindi katika dakika ya 65, na kuiacha City pointi 3 pekee nyuma ya Arsenal huku wakiwa na mechi moja mkononi.
Katika mechi ambapo kila timu ilibuni nafasi za ufungaji, kiungo Rayan Cherki alionyesha weledi wake wa chenga, na kuwapita mabeki wa Arsenal kuikweka City kileleni.
Hata hivyo, Kai Havertz alimshinikiza kipa Gianluigi Donnarumma kufanya makosa na kuirejesha Arsenal mchezoni chini ya dakika 2 baadaye.
Arsenal yake Mikel Arteta, ilipoteza nafasi kadhaa baadaye likiwemo jaribio la Eberechi Eze lililogonga mlingoti, na kichwa cha Havertz kilichopaa centimita kadhaa juu ya mtambaa panya katika dakika za mwisho, na kujipalia makaa wanapoandamwa na vijana wa Pep Guardiola.
Katika matokeo mengine, Liverpool walihitaji kichwa cha nahodha wao Virgil Van Dijk, kupata ushindi katika dakika ya 100 na kuweka hai matumaini ya kufuzu dimba la klabu bingwa bara Ulaya.
Mechi hiyo dhidi ya Everton ilisalia sare ya 1-1 katika muda wa kawaida, ila Van Dijk akawapa matumaini katika dakika za majeruhi.
Wakati uo huo, masaibu ya Chelesea yaliongezeka, wakifikisha rekodi ya kichapo cha mechi 4 za ligi mfululizo bila kufunga bao, walipocharazwa bao 1-0 na Manchester United.
Kwa sasa, Arsenal wangali kileleni na pointi 70 baada ya mechi 33, huku City wakifuata na pointi 67 kutokana na mechi 32.
Manchester United ni wa tatu kwa pointi 58, alama sawa na Aston Villa, na alama 3 mbele ya Liverpool walio katika nafasi ya 5.
Chelsea wanashikilia nafasi ya 6 wakiwa na pointi 48, wakitoshana pointi na Brentford na Bournemouth.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 










































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































