SHUJAA WAPANGWA KUNDI GUMU BAADA YA HONG KONG
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji 7 kila upande, Shujaa, imepangwa katika kundi jingine linaloonekana gumu katika mkondo ujao wa ubingwa wa SVNS duniani jijini Valladolid, utakaosakatwa tarehe 29-31 mwezi ujao.
Shujaa watamenyana na Afrika Kusini, Australia, na Uingereza kwenye Pool A, na wataelekea kwenye mkondo huo baada ya kumaliza katika nafasi ya 7 kwenye mkondo wa kwanza wa Hong Kong hapo jana ulioweka wazi udhaifu wao hasa katika safu ya ulinzi na ukosefu wa makali katika mashambulizi.
Dhidi ya Afrika Kusini, Kenya ilidhihirisha uwezo wake wa kupambana katika mashindano ya kiwango cha juu, licha ya kichapo chembamba cha 26-22 katika awamu ya robo fainali jijini Hong Kong.
Hata hivyo, Australia inasalia changamoto kubwa kwa Kenya, ikiiadhibu 14-5 katika mechi ya ufunguzi ya mkondo wa Hong Kong, na kuweka wazi masaibu ya Kenya katika safu ya ulinzi na kuvuruga mashambulizi yao.
Mechi inayoonekana nyepesi kwa Shujaa ni dhidi ya Uingereza, ambayo ilimaliza chini ya Kenya katika mkondo wa Hong Kong, na licha ya kutokutanishwa katika mkondo huo, Kenya imekuwa na rekodi nzuri dhidi yake katika mashindano ya awali.
Kenya ilianza vibaya mkondo huo kwa kupoteza mechi 2 za ufunguzi kabla ya kunguruma dhidi ya Marekani na kutinga robo fainali.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 










































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































