BRIGHTON YAIDUWAZA CHELSEA EPL
Timu ya Brighton iliikalifisha Chelsea kwa kichapo cha mabao 3-0 na kuiruka kwenye msimamo wa jedwali la ligi kuu nchini Uingereza, EPL, na hivyo kuweka hai matumaini ya kushiriki michezo ya bara Ulaya msimu ujao huku ikimpalia makaa meneja wa Chelsea Liam Rosenior.
Mabao ya Ferdi Kadioglu, Jack Hinshelwood na Danny Welbeck yaliipandisha Brighton hadi katika nafasi ya 6, Chelsea nao wakiandikisha rekodi ya kupoteza mechi 5 za ligi mfululizo bila kufunga bao kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1912.
Seagulls waliilemea the Blues kwa misururu ya makombora, the Blues wakiandikisha shoti moja pekee lililolenga bao katika mechi nzima.
Kwa sasa Chelsea wameshuka hadi nafasi ya 7 kwa pointi zao 48, wakiwa pointi 3 pekee mbele ya Everton katika nafasi ya 10, matumaini yao ya kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao yakianza kudidimia.
Tayari mkufunzi Rosenior yuko chini ya shinikizo, mashabiki uwanjani jana wakianza kuimba nyimbo za kumtaka aondoke.
Leo usiku, Manchester City wana fursa ya kumwangusha ndovu kwa mara ya kwanza msimu huu, watakapoingia dimbani dhidi ya Burnley.
Ushindi kwa City utawafikisha pointi 70 sawa na Arsenal, ila huenda wakawa juu kutokana na tofauti ya mabao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 










































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































