#Football #Sports

JUNIOR STARLETS WAWADHALILISHA WAGENI, KUPAMBANA NA UGANDA

Timu ya taifa ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17, Junior Starlets, itamenyana na wenzao wa Uganda katika raundi ya pili ya mashindano ya kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya kombe la dunia kwa chipukizi, FIFA World Cup U17 Women.

Hii ni baada yao kukosa adabu ya mwenyeji na kuidhalilisha Namibia kwa kichapo cha mabao 5-0 ugani Ulinzi Sports Complex katika mkondo wa pili, na kufikisha ushindi wa jumla ya mabao 7-1 kufuatia ushindi wa mabao 2-1 katika mkondo wa kwanza.

Wakiwa tayari mbele kutokana na ushindi kwenye mkondo wa kwanza jijini Windhoek, Starlets waliingia katika mechi ya Jumamosi wakilenga kuidhibiti ili kusalia kileleni.

Lengo lao lilifanikiwa ila mabao yakasubiri hadi kipindi cha pili ambako mifereji ya mabao ilifunguliwa.

Brenda Achieng aliongoza maangamizi, akifunga mara 3 katika dakika za 46, 69 na 82 na kuonyesha uweledi wake mbele ya lango.

Mabao mengine yalifungwa na Emily Adhiambo kunako dakika ya 54 na Elizabeth Alizeba katika dakika za majeruhi.

Kwa sasa chipukizi hao wanajiandaa dhidi ya Uganda katika raundi ya pili, mechi zitakazochezwa kwa mikondo mwili kati ya tarehe 22 na 31 mwezi ujao.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *