#Sports

CITY WAPAA JUU YA ARSENAL, WAISHUSHA BURNLEY

Timu ya Manchester City imepanda kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya soka nchini Uingereza kwa mara ya kwanza tangu wikendi ya ufunguzi wa ligi msimu huu, na kuishusha Arsenal hadi katika nafasi ya pili.

Vijana hao wa Pep Guardiola walipanda kileleni baada ya kuilaza Burnley bao 1-0 kupitia kwa mshambulizi wao Erling Haaland kunako dakika ya 5, na licha ya nafasi nyingi za wazi walizobuni ikiwemo mashuti 27, hawakufanikiwa kufunga zaidi ya mara moja.

Ushindi huo pia uliizamisha Burnley, ambayo imejiunga na Wolves kuwa miongoni mwa timu 2 ambazo zimeshushwa daraja msimu huu.

City na Arsenal wana pointi 70 kila mmoja baada ya mechi 33, wakiwa na ubora sawa wa mabao, ila City wako kileleni kutokana na mabao 66 waliyofunga huku Arsenal wakifunga mabao 63 kufikia sasa.

Vigogo hao wamesalia na mechi 5 kabla ya msimu kukamilika, ligi hiyo ikishuhudia ushindani mkali ambapo Arsenal wanalenga ubingwa ambao umewakwepa kwa miaka 22, nao City wakilenga ubingwa mara ya 7 katika misimu 9 chini ya Guardiola.

Wakati uo huo, Burnley walio na pointi 20 pekee katika mechi 34, watahitaji kujipanda upya katika ligi ya Championship msimu ujao.

Kwingineko, juhudi za Bournemouth kufuzu soka ya bara Ulaya zilipigwa breki jana usiku, baada ya Sean Longstaff kuisawazishia Leeds katika dakika ya 97 na kufanya mambao kuwa mabao 2-2.

Sare hiyo imewainua Leeds pointi 9 juu ya eneo la kushushwa daraja, kinyang’anyiro kikisalia kati ya West Ham, Tottenham na Nottingham kuhusu ni nani atakayejiunga na Wolves na Burnley kuiaga EPL mwishoni mwa msimu.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *