K’OGALO WAKAMATA USUKANI WA KPL
Bingwa wa kihistoria wa ligi kuu ya soka nchini, KPL, Gor Mahia, waliongeza pengo la pointi kileleni mwa jedwali la ligi hiyo na kushika usukani, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao AFC Leopards katika debi la mashemeji.
Baada ya ukame wa mabao kwa pande zote licha ya K’Ogalo kutamalaki mchezo, bao Alpha Onyango lilitatua kesi ya mashemeji na kuwapandisha Gor hadi pointi 61, 6 mbele ya Ingwe.
Licha ya ushindi mwembamba, Gor waliambulia pointi 3 muhimu, ambazo huenda zikatoa mwelekeo wa ligi hiyo ambayo sasa imesalia na mechi 5 pekee.
Leopards sasa watalazimika kunoa kucha zao wanaporejea mawindoni kusaka ubingwa wa kwanza wa ligi hiyo tangu mwaka wa 1998.
Wanasalia katika nafasi ya pili kwa pointi 55.
Katika matokeo mengine, vita vya kujinasua kutoka eneo la kushushwa daraja vilishika kasi kati ya Kariobangi Sharks na APS Bomet, timu hizo mbili zikiandikisha ushindi.
APS walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sofapaka, nao Sharks wakiandikisha ushindi sawa dhidi ya Murang’a Seal.
Bandari FC walikubali kichapo cha mabao 2-1 mikononi mwa wanajeshi wa Ulinzi Stars, nao Nairobi United wakapata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mathare United.
Shabana na Kenya Police waliachana kwa sare tasa.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 
































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































