SAWE AVUNJA REKODI YA MARATHON
Mkenya Sebastian Sawe amekuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za marathon chini ya muda wa saa mbili, baada ya kuibuka bingwa wa mbio za London Marathon katika muda wa 1:59:30.
Kwa upande wa wanawake, Tigst Assefa wa Ethiopia alitetea taji lake la mbio za London Marathon, na kuvunja rekodi yake ya awali.
Hata hivyo, gumzo kubwa lilimhusu Sawe katika mbio hizo za jana, baada ya kuandikisha historia hiyo kwa kuvunja rekodi iliyowekwa na mkenya mwenzake marehemu Kelvin Kiptum, aliyeweka rekodi ya muda wa 2:00:35 katika mbio za Chicago Marathon mwaka wa 2023.
Sawe mwenye umri wa miaka 31 ambaye hajawahi kushindwa katika mbio za marathon, alivunja rekodi hiyo kwa sekunde 65.
Yomif Kejelcha wa Ethiopia alimwandama Sawe kwa kipindi kirefu cha mbio hizo kabla ya kunyong’onyea na kumaliza wa pili kwa muda wa 1:59:41, huku Jacob Kiplimo wa Uganda akijinyakulia shaba kwa muda wa 2:02:28, wote 3 wakimaliza chini ya muda ulioandikishwa na Kiptum.
Wakati uo huo, bingwa mtetezi katika mbio za wanawake Assefa aliteteta taji lake katika muda wa 2:15:41, mbele ya wakenya Hellen Obiri na Joyciline Jepkosgei.
Waswizi Marcel Hug na Catherine Debrunner walishinda mbio za viti vya magurudumu katika mashindano ya wanaume na wanawake mtawalia.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 
































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































