WAFCON 2026 YAAHIRISHWA
Dimba la taifa bingwa barani Afrika la wanawake mwaka huu, WAFCON 2026 limeahirishwa, zikiwa zimesalia siku 11 kabla ya tarehe iliyokuwa imeratibiwa kuanza kwa mashindano hayo.
Kupitia taarifa, shirikisho la soka barani Afrika, CAF, limesema Makala ya mwaka huu yataandaliwa mwezi Julai kutokana na kile ambacho limetaja kwamba sababu zisizoweza kutabirika.
Makala ya mwaka huu ambayo pia yalifaa kutumiwa kufuzu kwa kombe la dunia la wanawake nchini Brazil baadaye mwaka huu, yalikuwa yamepangwa kuanza tarehe 17 mwezi huu na kukamilika tarehe 3 mwezi ujao.
Tayari timu ya taifa ya wanawake, Harambee Starlets, imekuwa kwenye maandalizi ya mwisho ughaibuni.
WAFCON 2026 ilikuwa imeratibiwa kuandaliwa nchini Morocco kwa mara ya 3 mfululizo, ingawa tetesi za taifa hilo kukosa utayari wa kuwa mwenyeji zilizuka baada ya vurugu kushuhudiwa kwenye fainali za dimba la AFCON 2025.
Kuahirishwa kwa dimba hilo kunaibua maswali kuhusu kujitolea kwa CAF kwa mashindano ya wanawake, hasa baada ya Makala ya mwaka wa 2020 kufutiliwa mbali kutokana na janga la Covid-19, nayo ya mwaka 2024 ikilazimika kuahirishwa hadi mwaka jana kutokana mkanganyiko wa ratiba ikiwemo mashindano ya Paris Olympics 2024.
Mashindano ya CHAN mwaka jana pia yaliahirishwa dakika za mwisho, zikiwa zimesalia siku 18 pekee na kuandaliwa Agosti mwaka jana.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 
































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































