#Football #Sports

ASTON VILLA WAONJESHWA KICHAPO EUROPA

Bao la Chris Wood liliipa Nottingham Forest uongozi muhimu katika mechi ya mkondo wa kwanza wa semi fainali ya kombe la UROPA dhidi ya Aston Villa jana usiku.

Wood alifunga bao hilo kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 71 baada ya Lucas Digne kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, bao hilo likimaanisha vijana wa Vitor Pereira wataingia mkondo wa pili Alhamisi ijayo ugani Villa Park wakiwa na uongozi wa bao 1-0.

Villa waliilaza Forest mabao 3-1 ugani humo mwezi Januari katika mechi ya ligi kuu, EPL, ila watahitaji kazi ziada ili kubatilisha kichapo cha jana mkufunzi wao Unai Emery anaposaka taji la 5 la UROPA.

Katika semi fainali nyingine, Braga waliandikisha ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi Freiburg, na washindi wa semi fainali hizo watakutana kwenye fainali mwezi ujao.

Kwenye ligi ya Conference, Crystal Palace iliweka hai matumaini yake ya kunyakua kombe hilo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Shakatar Donetsk huku Rayo Vallecano wakipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Strasbourg.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *