ROONEY ONYANGO APATA AFUENI
Jopokazi la kushughulikia mizozo ya michezo, SDT, limemwondolea marufuku ya muda beki wa Harambee Stars Rooney Onyango, aliyokuwa amewekewa na shirika la kukabili matumizi ya dawa za kutitimua misuli nchini, ADAK.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 24 anayesakata soka ya kulipwa katika klabu ya Sogndal Fotball nchini Norway, alikuwa ametemwa tarehe 28 mwezi jana, akishutumiwa na kosa la kutopatikana kwa vipimo.
Kulingana na ADAK, Onyango alikosa mara tatu kutoa vipimo ndani ya kipindi cha miezi 12, kosa linaloweza kusababisha marufuku ya miaka 2 chini ya sheria za kudhibiti matumizi ya dawa hizo.
Hata hivyo kwenye uamuzi wake wa hapo jana, SDT ilitoa amri ya kufutilia mbali marufuku hiyo ya muda hadi malalamishi ya pande zote yatakaposikilizwa na kuamuliwa.
Uamuzi huo sasa unamwezesha kushiriki shughuli zote za kandanda kwa klabu na taifa kesi dhidi yake inaposubiri uamuzi.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 10 mwezi huu.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































