#Football #Sports

GOR WAKANYAGA GWARIDE KUELEKEA UBINGWA

Viongozi wa ligi kuu ya soka nchini, KPL, Gor Mahia, waliendelea na msafara wao wa kuelekea ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wanajeshi wa Ulinzi Stars hapo jana.

Green Commandos walivunja ngome ya Ulinzi ndani ya dakika 9 za kwanza, Enoch Morrison akifunga kupitia mkwaju wa penalti baada ya Musa Shariff kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Licha ya jeraha kwa beki Sylvester Owino mwishoni mwa kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mike Kibwage, Gor Mahia waliendelea kutamalaki mchezo, nguvu mpya Patrick Essombe wa Cameroon akiongeza uongozi wa vijana wake Charles Akonnor katika dakika ya 65.

Shariff Musa baadaye alifunga bao lake mwenyewe, na kufanya mambo kuwa 3-0 kabla ya Stephen Odhiambo kuwafuta machozi wanajeshi ambao sasa wamekita kambi katika eneo la kushushwa daraja.

Ushindi huo unawafikishia Gor pointi 53, pointi 10 mbele ya wapinzani wao AFC Leopards.

Leopards walizimwa Jumamosi na klabu ya Mathare United kwa kichapo cha mabao 4-1, na kumlazimu mwenyekiti wa klabu hiyo Boniface Ambani kuomba msamaha kwa mashabiki.

Katika matokeo mengine, Kariobangi Sharks waliwakabidhi Shabana FC kichapo cha pili mfululizo, baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 2-1 ugani Gusii Stadium

Shabana wamesalia katika nafasi ya 3 na pointi 40, pointi 2 mbele ya Kakamega Homeboyz wanaofuatiwa na na Murang’a Seal na kisha bingwa mtetezi Police FC.

Tusker ambao sasa wameingia kwenye msururu wa ushindi, wanashikilia nafasi ya 7, wakiwa pointi 3 pekee nyuma ya nambari 3.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *