#Football #Sports

CITY YAHARIBIWA, KISA CHA BODØ KIKITAMATIKA UEFA

Kadi nyekundu kwa nahonda wa Manchester City Bernardo Silva katika dakika ya 20 ilitoa mwelekeo wa mechi ya mkondo wa pili ya raundi ya 16 ya dimba la klabu bingwa bara Ulaya, mabao mawili ya Vinicius Jr yakiihakikishia Real Madrid ushindi wa mabao 2-1 jana usiku.

Real walifuzu robo fainali kwa jumla ya mabao 5-1 kutokana na ushindi wa mabao 3-0 katika mkondo wa kwanza.

Licha ya Man City kusalia 10 uwanjani kwa zaidi ya dakika 70, walivamia lango la Real zaidi ya mara 20, ila shoti moja pekee ikawa bao baada ya Erling Haaland kufunga bao ambalo baadaye liliishia kuwafuta machozi.

Kwa sasa Real yake Alvaro Arbeloa, imewabandua Manchester City wake Pep Guardiola mara 3 mfululizo katika mashindano hayo.

Wakati uo huo, kisa cha Bodo/Glimt kuwaangusha miamba wa soka bara Ulaya kilitamatika kwa machozi jana usiku jijini Lisbon, Ureno.

Kabla ya mechi hiyo, Bodo walikuwa na jukumu la pekee la kulinda uongozi wao wa mabao 3-0 waliyofunga katika mkondo wa kwanza, ila mashambulizi baada ya mashambulizi ya wenyeji wao Sporting CP yaliigeuza Bodo kuwa nyumba ya udongo, ambayo haingeweza kustahamili vishindo.

CP walifunga mabao 3 katika muda wa dakika 90 na kulazimisha muda wa ziada ambapo walifunga mabao mengine 2 na kufikisha jumla ya mabao 5-3.

Glimt walikuwa gumzo kwenye mashindano hayo baada ya kuwanyuga miamba kadhaa ikiwemi kuibandua Inter Milan katika awamu ya mwondoano.

Hata hivyo, mbawa zao zilikatwa hapo jana na CP, ingawa wataondoka kwa Fahari.

Katika mashindano mengine, Chelsea watabaki kujiuliza kilichowatendekea, baada ya kubebeshwa mzigo wa jumla ya mabao 8-2 na bingwa mtetezi PSG.

Baada ya kichapo cha mabao 5-2 katika mkondo wa kwanza nchini Ufaransa, PSG walianzia walikoachia walipofika Uingereza, na kuwadhalilisha wenyeji wa kwa kichapo kingine cha mabaoa 3-0

Arsenal walijikatia tiketi ya robo fainali kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bayer Leverkusen, na kufikisha jumla ya mabao 3-1.

Mechi za mkondo wa mwisho zitachezwa leo usiku- Newcastle watakuwa wageni wa Nou Camp dhidi ya Barcelona, Tottenham waialike Atletico Madrid, Bayern dhidi ya Atalanta na kisha Liverpool dhidi ya Galatasaray.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *