TIMU ZA KPL KUMENYANA SEMI FAINALI YA FKF CUP
Klabu ya Police FC itachuana na Bandari FC kwenye awamu ya nusu fainali ya kombe la FKF kufuatia ushindi wa klabu hizo mbili katika awamu ya robo fainali.
Bao la pekee la mchezo la Abud Omar kupitia ikabu liliwapa maafande hao ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Shabana FC na kuwapa tiketi ya nusu fainali.
Kwa upande wao, Bandari FC waliopoteza uongozi mara mbili katika kipindi cha kwanza dhidi ya Mfalme, walifanikiwa kufunga mabao mawili katika kipindi cha pili na kuambulia ushindi wa mabao 5-2 katika pambano la kukata na shoka.
Semi fainali nyingine itawakutanisha KCB FC na Tusker FC.
Nguvu mpya Ibrahim Joshua aliifungia Tusker bao la ushindi katika dakika za lala salama na kufanya mambo kuwa mabao 2-1 dhidi ya Ulinzi.
Nao KCB waliwabwaga mabingwa watetezi wa kombe hilo Nairobi United, kwa kichapo cha bao 1-0 na kuhakikisha kuwa kombe hilo linapata bingwa mpya mwezi ujao.
Mechi za nusu fainali zitachezwa tarehe 16 na 17 mwezi huu, washindi wakikutana kwenye fainali tarehe 14 mwezi ujao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































