ARSENAL WAKATA KIU YA MIAKA 20 UEFA
Timu ya Arsenal ilikata tiketi ya kuingia fainali za kombe la klabu bingwa bara Ulaya kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 20, baada ya bao la Bukayo Saka kuwapa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid kwenye semi fainali jana usiku.
Timu hizo zilikutana kwa marudiano kwenye mkondo wa pili kufuatia sare ya bao 1-1 katika mkondo wa kwanza, na licha ya tahadhari na mashambulizi ya kushtukiza, ni the Gunners waliopata mpenyo kupitia wing’a huyo kunako dakika ya 44.
Mara ya mwisho kwa vijana hao wa Mikel Arteta kucheza fainali ya klabu bingwa bara Ulaya ulikuwa mwaka wa 2006, ambako walizimwa na Barcelona.
Kwa sasa kizingiti kati yao na taji la kwanza la kombe hilo ni bingwa mtetezi PSG au Bayern Munich, watakaomenyana leo usiku kwa mechi ya marudiano ili kumtuma atakayepambana na Arsenal kwenye fainali.
Klabu hiyo sasa iko katika nafasi nzuri ya kutawazwa mabingwa wa ligi kuu ya soka EPL ambayo wanaongoza, na kombe hilo ambalo fainali yake itaandaliwa jijini Budapest, nchini Hungary, mwishoni mwa mwezi huu.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































