#Football #Sports

TUSKER FC, NAIBOIS KUVAANA KPL

Jumla ya mechi nne za ligi kuu ya soka nchini, KPL, zimeratibiwa kusakatwa hii leo ligi hiyo inapokaribia ukingoni.

Mechi hizo zilizofaa kusakatwa wikendi iliyopta, ziliahirishwa kutokana na awamu ya robo fainali ya kombe la FKF.

Katika uwanja wa Police Sacco, wenyeji Kenya Police wataikaribisha Murang’a Seal wakilenga kulipiza kisasi kufuatia kichapo cha bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza.

Police wataingia katika mechi ya leo wakiwa wamesakata mechi 7 bila kupoteza katika mashindano yote, wakifungwa bao moja pekee kwenye msururu huo.

Kwa upande wao, Murang’a Seal wako katika mwanguko, wakikosa kuandikisha ushindi katika mechi 7 zilizopita, hatua iliyosababisha kutimuliwa kwa kocha mkuu Osborne Monday.

Mechi zingine zitawakutanisha Nairobi United dhidi ya Tusker FC ugani Ulinzi Sports Complex, Naibois wakiingia mechi ya leo wakiuguza kichapo cha kubanduliwa nje ya kombe la FKF wikendi iliyopita dhidi ya KCB FC.

Kabla ya kichapo hicho, Naibois walikuwa wameandikisha ushindi mara 4 katika mechi 5, na kutoka sare mara moja.

Wapinzani wao Tusker wamekuwa katika hali tete, wakipoteza mara 3 katika mechi 5 zilizopita za ligi.

Mechi nyingine itashuhudia Bandari FC wakichuana na Posta Rangers, Bandari wakiwa na ujasiri hasa baada ya kutinga semi fainali za kombe la FKF.

APS Bomet wataikaribisha KCB FC katika mechi nyingine.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *