#Rugby #Sports

KENYA CUP: KABRAS RFC WAMALIZA KILELENI

Klabu ya Kabras RFC ilidhihirisha ubabe wao katika mchezo wa raga nchini kwa kuandikisha ushindi wa 27-13 dhidi ya Menengai Oilers ugani ASK Grounds mjini Kakamega, na kumaliza kileleni mwa msimu kawaida katika ligi ya Kenya Cup.

Ushindi huo uliwafikishia pointi 52 kileleni kutokana na mechi 11, pointi 2 mbele ya KCB RFC.

Timu hizo mbili za kwanza zimejikatia tiketi ya kushiriki semi fainali za nyumbani moja kwa moja, nao Oilers wakijikatia tiketi ya kushiriki playoff baada ya kumaliza katika nafasi ya 3 wakiwa na pointi 45.

Kwa sasa Kabras ambao ni mabingwa watetezi, wamecheza mechi 52 bila kupoteza, mkufunzi wao Carlos Katywa naye akifikisha mechi 50 bila kupoteza tangu achukue uongozi wa klabu hiyo.

Katika matokeo mengine, KCB RFC waliandikisha ushindi wa 57-17 dhidi ya Daystar Falcons, Strathmore Leos wakipata fursa ya kushiriki playoff kutokana na ushindi wa 32-10 dhidi ya Harlequin.

Nakuru RFC waliicharaza MMUST 25-19, nao Impala wakaimarisha juhudi zao za kuepuka kushushwa daraja kwa kuwacharaza Nondescripts 17-13.

Licha ya ushindi wa 9-8 wa Kisumu RFC dhidi ya KU Blak Blad, hawakufanikiwa kukwepa shoka la kushushwa daraja baada ya kumaliza katika nafasi ya 11, MMUST wakimaliza wa mwisho ingawa wana afueni kutokana na mechi yao iliyoahirishwa.

Playoff zitachezwa Aprili 18, kisha semi fainali Aprili 25 kabla ya fainali Mei 2.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *