#Football #Sports

NEYMAR, ROBINHO JR WAPATANA HADHARANI KUFUATIA KOFI

Nguli wa soka nchini Brazil Neymar Jr amemwomba msamaha hadharani mchezaji mwenza wa klabu ya Santos Robinho Junior baada ya kumzaba kofi kinda huyo wakati wa mazoezi.

Klabu ya Santos ilisema kwamba imeanzisha uchunguzi kufuatia makabiliano kati ya Neymar na Robinho Junior, ambaye ni mwanawe mshambulizi wa zamani wa klabu ya Real Madrid na Manchester City.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Brazil, ugomvi ulizuka kwa sababu Neymar ambaye ndiye mfungaji bora zaidi wa timu ya taifa ya Brazil, hakufurahishwa alipopigwa chenga na kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 walipokuwa mazoezini Jumapili iliyopita.

Robinho Jr alithibitisha siku ya Jumanne baada ya mechi ya Sudamericana kwamba Neymar alimzaba kofi, ila akasema suala hilo lilikuwa limetatuliwa.

Wakati wa mechi hiyo, Neymar alifunga bao la Santos kwenye sare ya bao 1-1 na kumpiga pambaja Robinho waliposherehekea bao hilo.

Licha ya changamoto za majeraha, Neymar mwenye umri wa miaka 34, anatarajiwa kujumuishwa kikosi na kocha wat imu ya taifa Carlo Ancelotti kwa kombe la dunia mwezi ujao.

Naye Robinho mwenye umri wa miaka 42 aliyewahi kucheza Pamoja na Neymar katika klabu ya Santos, anatumikia kifungo nchini Brazil baada ya kuhukumiwa kwa makosa ya ubakaji nchini Italia.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *