#Football #Sports

GOR WAPIGWA JEKI LIGINI WANAPOSAKA UBINGWA

Viongozi wa ligi kuu ya soka nchini, KPL, Gor Mahia, wamepigwa jeki katika juhudi zao za kusaka ubingwa wa ligi hiyo msimu huu, kufuatia kurejea kwa mshambulizi wao Felix Mboya aliyekuwa amekaa nje kwa muda mrefu kutokana na jeraha.

Mshambulizi huyo wa timu ya taifa Harambee Stars amekuwa nje kwa miezi kadhaa baada ya kufanyiwa upasuaji kurekebisha tatizo la mara kwa mara la goti lililokuwa limetishia kukatiza msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo.

Mshambulizi huyo wa zamani wa Posta Rangers, alifanyiwa upasuaji mwezi Machi, akiratibiwa kusalia mkekani kwa wiki 12 hadi mwisho wa msimu.

Hata hivyo, Mboya ameonyesha kupona upesi na kurejea kikosini Gor Mahia wanapojiandaa kwa mechi zilizosalia kabla ya kutamatika kwa msimu.

Kupitia taarifa kwenye mitandao ya kijamii, Gor Mahia amethibitisha kurejea kwa fowadi huyo na kumwalika arejee mazoezini.

Mboya aliyejiunga na Gor mwanzoni mwa msimu, alikuwa amefunga mabao 7 katika mechi 17 kabla ya upasuaji huo, akiwa bado ndiye mfungaji bora wa timu hiyo hadi sasa.

Klabu hiyo inaongoza ligi ya KPL ikiwa na pointi 64, 9 mbele ya mahasimu wao AFC Leopards.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *