GUARDIOLA AHOFIA UCHOVU KABLA YA FAINALI
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema ana matumaini kikosi chake kitaweza kushinda uchovu kinapoikabili Chelsea FC katika fainali ya Kombe la FA siku ya Jumamosi.
Manchester City bado wanapambana kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Arsenal FC, lakini kwa sasa macho yao yataelekezwa Wembley wakisaka kutwaa taji la pili la nyumbani msimu huu.
City walicheza dhidi ya Crystal Palace Jumatano na watarudi tena dimbani siku tatu baada ya fainali hiyo watakapomenyana na Bournemouth kwenye ligi kuu.
RATIBA YA EPL WIKIENDI HII
Ligi Kuu England itaendelea wikiendi hii kwa michezo kadhaa muhimu ya duru ya 37 msimu huu. Leo usiku, Aston Villa watawakaribisha Liverpool FC katika mchezo wa saa nne usiku.
Jumapili, Manchester United watavaana na Nottingham Forest saa nane na nusu mchana huku Newcastle United wakimenyana na West Ham United usiku. Mechi nyingine zitazikutanisha Brentford FC dhidi ya Crystal Palace, Leeds United dhidi ya Brighton & Hove Albion pamoja na Everton FC dhidi ya Sunderland AFC.
Duru hiyo itahitimishwa Jumatatu na Jumanne ambapo Arsenal FC watacheza na Burnley FC kabla ya Manchester City kuvaana na AFC Bournemouth huku Chelsea FC wakikabiliana na Tottenham Hotspur.
Imetayarishwa na Cyrus Sifuna
English 













































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































