MAN CITY WAWATIA ARSENAL KWENYE TANURI NA KICHAPO KWA PALACE
Manchester City waliandikisha ushindi rahisi wa mabao 3-0 dhidi ya Crystal Palace licha ya kocha mkuu Pep Guardiola kukichezesha kikosi cha akiba, na kuwatia viongozi wa EPL, Arsenal kwenye tanuri la moto.
Guardiola alifanya mabadiliko 6 ya kikosi kilichowalaza Brentford mabao 3-0 wikendi iliyopita, na kuwaacha nje wachezaji wake mahiri kama vile Erling Haaland, Jeremy Doku na Rayan Cherki.
Phil Foden alikuwa chanzo cha maangamizi dhidi ya Palace, mwanzo akawahadaa mabeki kwa kisigino na kummegea pasi Antoine Semenyo katika bao la ufunguzi, kabla ya kumwandalia Omar Marmoush bao la pili katika kipindi cha kwanza.
Nguvu mpya Rayan Cherki alimwandalia kinda wa Brazil Savino aliyefunga bao la 3 katika kipindi cha pili, na kuweka hai matumaini ya the Cityzens kupelekana na Arsenal mguu kwa mguu hadi mechi ya mwisho kuamua ubingwa.
Ushindi wa City ulipandishia pointi hadi 77, 2 pekee nyuma ya Arsenal huku kila timu ikisalia na mechi 2 kabla ya mwisho wa msimu.
City wanajiandaa kwa fainali ya kombe la FA Jumamosi hii dhidi ya Chelsea, wakilenga kushinda mataji matatu ya nyumbani katika msimu ambao wamekuwa vuguvugu.
Palace waliowabandua City kwenye fainali ya FA msimu jana, wako katika nafasi ya 15, wanapojiandaa kwa fainali ya Conference League dhidi ya Rayo Vallecano.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































