GOR WALAZIMISHA SARE, LEOPARDS WAPIGWA JEKI
Timu ya Gor Mahia ilipigwa breki katika safari ya kunyakuwa ubingwa wa 22 wa ligi kuu ya soka, KPL, kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya bingwa mtetezi, Police FC, na kuwapa matumaini AFC Leopards wanaoemezea mate taji hilo.
Leopards walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mara Sugar, na sare ya Gor ikipunguza mwanya wa pointi kati yao hadi 7 huku Leopards wakisalia na mechi moja zaidi ya wenzao.
K’Ogalo waliokuwa wakikodolewa macho na kichapo, walifanikiwa kunusuru pointi katika dakika za lala salama kupitia kwa nguvu mpya Ebenezer Assifuah, baada ya Brian Chonjo kuwaweka Police FC mbele kunako dakika ya 22.
Kwa sasa Gor wana pointi 65 kileleni baada ya kusakata mechi 31, nao Ingwe wakiwaandamana katika nafasi ya 2 baada ya mechi 30.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































