GUARDIOLA: SIJAWAHI KUWA NA IMANI NA VAR
Kocha mkuu wa Manchester City Pep Guardiola, amesema hajawahi kuamini chochote katika marefa wa EPL na msaidizi wa refa kupitia video, VAR, akirejelea uamuzi wa kuipokonya West Ham United bao la kusawazisha dhidi ya Arsenal Jumapili iliyopita.
Arsenal waliongeza pengo la pointi kati yao na City hadi 5 kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya the Hammers, ambao walinyimwa bao la kusawazisha katika muda wa majeruhi baada ya refa kulazimika kutumia VAR ambapo alitazama marudio ya tukio hilo mara 17 kabla ya kufuta bao la West Ham.
Hata hivyo, City wana fursa ya kupunguza pengo hilo hadi pointi 2 watakapoialika Crystal Palace leo usiku ugani Etihad kucheza mechi yao ya mkononi.
Hata hivyo, Guardiola amesema matokeo ya mechi hiyo yatategemea mia kwa mia mchezo wa wachezaji wake na wala si uamuzi wa refa.
Akizungumza na wanahabari kuhusu kinyang’anyiro kati yake na Arsenal, Guardiola amesema lengo lake ni kwa mechi dhidi ya Palace kabla ya kuangazia nyingine, akisisitiza kuwa kupoteza makini kunaweza kuitumbukiza timu katika hali ngumu.
Crystal Palace wako katika nafasi ya kuamua mwelekeo wa ligi hiyo, ikizingatiwa kuwa wana mechi dhidi ya vigogo hao Arsenal na City, ingawa pia wanajiandaa kwa fainali ya Conference League.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































