KIVUMBI CHA FKF CUP
Jumla ya timu nne zitashuka dimbani hapo kesho kuwania nafasi ya kufuzu fainali ya kombe la FKF, mechi zote 2 zikiratibiwa kusakatwa katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.
Katika semi fainali ya kwanza, Tusker FC walioshinda kombe hilo mara ya mwisho msimu wa 2021-22, watapambana na KCB FC huku Tusker wakipigiwa upato wa kunyakua kombe hilo.
Mechi hiyo itaanza saa saba mchana.
Semi fainali nyingine itashuhudia Police FC wakifyetua bahati ya kutinga fainali watakapovaana na Bandari FC, majira ya saa kumi kasorobo ugani Nyayo.
KCB ndiyo timu ya pekee iliyosalia katika kinyang’anyiro hicho, ambayo haijawahi kushinda taji la FKF Cup, Bandari wakiwa mabingwa wa mwaka 2019, Kenya Police pia wakishinda mara moja ambao ni mwaka wa 2024.
Tusker ambao wanashikilia nafasi ya 7 katika jedwali la ligi kuu KPL, wamekuwa na changamoto tele msimu huu, wakilazimika kumtimua kocha mkuu Charles Okere.
Kocha mkuu wa sasa Julien Mette, amewataka vijana wake kusalia watulivu wanapolenga kujifariji na kombe hilo baada ya matumaini ya kunyakua ubingwa wa KPL kunyauka.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































