#Football #Sports

WOLVES WAIAGA EPL NA NYUNDO YA WEST HAM

Klabu ya Wolves imekuwa ya kwanza kushushwa daraja kutoka ligi kuu ya soka nchini Uingereza, EPL, msimu huu, wakiratibiwa kushiriki ligi ya Championship msimu ujao.

Wolves walio katika nafasi ya mwisho kwenye jedwali la EPL, walipokezwa kichapo cha mabao 3-0 na Leeds Jumamosi, na sare ya kutofungana kati ya West Ham na Crystal Palace jana usiku ikawakatia tiketi vijana hao wa Rob Edwards.

Timu hiyo iliyokuwa imeratibiwa kushushwa daraja wikendi iliyopita, iliokolewa na washindani wao Tottenham waliotoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Brighton, na kupewa afueni kabla ya kulipiwa nauli ya kuelekea Championship na sare ya jana.

Wolves wameshiriki ligi kuu kwa miaka 8 iliyopita, na masaibu yao yalianza mapema msimu huu kabla ya wasimamizi kumleta mchezaji wake wa zamani Edwards mwezi Novemba katika juhudi za kuiokoa ila maji yakaendelea kuzidi unga.

Edwards aliwapata Wolves wakiwa wamecheza mechi 11 bila ushindi chini ya Vitor Pereira, na walikuwa na pointi 2 pekee.

Edwards alipoteza mechi zake 7 za kwanza kabla ya kuleta tumaini kwa kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Manchester United katika mechi ya mwisho ya mwaka wa 2025.

Licha ya matokeo bora katika mechi kadhaa ikiwemo sare dhidi ya Arsenal na kichapo kwa Liverpool na Aston Villa, mkondo wao ulikataa kubadilika, kwa sasa wakiwa na pointi 17 pekee baada ya mechi 33.

Licha ya kushushwa daraja, Wolves bado watakuwa na usemi kuhusu ni nani watakayeandamana naye kwenye safari hiyo, wakiikaribisha Tottenham wikendi hii.

Spurs wako katika nafasi ya 18, juu ya Burnley ambao pia wameonekana kuelekea kushushwa daraja.

Kinyang’anyiro cha kujiokoa sasa ni kati ya Leeds, Nottingham Forest, West Ham, Tottenham na Burnley, mambo kwa timu hizo mbili za mwisho yakiwa wazi kama mchana.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *