VILLA GUU MOJA SEMI FAINALI UROPA LEAGUE
Klabu ya Aston Villa itaingia katika mkondo wa pili wa mechi ya robo fainali ya dimba la UROPA League ikiwa na uongozi wa mabao 3-1 kufuatia ushindi wao hapo jana kwenye mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Bologna nchini Italia.
Baada ya kuponea awimbi ya mashambulizi kutoka kwa wenyeji wao, Villa walichukua uongozi kupitia bao la kichwa kutoka kwa Ezri Konsa mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kabla ya Ollie Watkins kuongeza la pili dakika ya 51.
Mshambulizi wa Uingereza Jonathan Rowe aliifungia Bologna bao la kufuta machozi katika dakika ya 90, ila Watkins akajibu haraka na kufanya mambo kuwa mabao 3-1, na kuipa timu hiyo ya Unai Emery ujasiri wanapoingia katika mkondo wa pili jijini Birmingham Alhamisi ijayo.
Villa wanaopigiwa upato kunyakua taji hilo na kuongeza idadi ya timu za Uingereza zitakazoshiriki dimba la klabu bingwa bara Ulaya msimu ujao, watalenga kumalizia kibarua nyumbani, ambako wamewalaza Bologna mara mbili tayari ndani ya miezi 18 iliyopita, kikiwemo kichapo cha mabao 2-0 msimu jana katika dimba la klabu bingwa bara Ulaya, na bao 1-0 mapema msimu huu.
Katika matokeo mengine, Nottingham Forest walitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Porto, Freiburg wakainyuga Celta Vigo mabao 3-0, huku Braga na Real Betis wakiachana kwa sare ya bao 1-1.
Katika mechi za Conference League, Crystal Palace waliweka hai matumaini ya kufuzu awamu ya nusu fainali kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fiorentina, matokeo sawa yakiandikishwa na Shakhtar Donetsk dhidi ya AZ Alkamaar, na Rayo Vallecano dhidi ya Athens huku Mainz wakiilaza Strasbourg mabao 2-0.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 











































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































