#Football #Sports

CITY WAFAIDI MASAIBU YA ARSENAL, WAILAZA CHELSEA

Manchester City walitumia fursa ya kuteleza kwa Arsenal katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa taji la ligi kuu ya Uingereza, EPL, kwa kuandikisha ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Chelsea ugani Stamford Bridge.

City walibomoa daraja la wenyeji wao kupitia kwa mabeki Nico O’Reily, Marc Guehi na wing’a Jeremy Doku katika kipindi cha pili, baada ya kipindi cha kwanza kutamatika kwa sare licha ya Chelsea kuonyesha ari ya kufunga.

Ushindi wao ulijiri siku moja baada ya viongozi Arsenal kurushiwa ganda la ndizi na AFC Bournemouth waliowapa kichapo cha mabao 2-1 uwanjani Emirates na kupoteza nafasi ya kuongeza pengo la alama kileleni.

City walianza kipindi cha kwanza wakiwa na mchezo usio wa kuridhisha, ila kiungo wao Rayan Cherki akatawala safu ya kati kwenye kipindi cha pili na kuchangia mabao mawili ya ufunguzi.

Ushindi huo sasa umeongeza pointi za vijana wa Pep Guardiola hadi 64, 6 nyuma ya vijana wa Mikel Arteta huku City wakiwa na mechi nyingine mkononi.

City wataialika Arsenal ugani Etihad Jumapili ijayo, huku Guardiola akisisitiza kuwa timu yake inafaa kuiheshimu Arsenal kwa kuonyesha umakini katika mechi hiyo.

Katika matokeo mengine, kocha mkuu wa Totenham Hotspur Roberto De Zerbi, alianza kibarua cha kuiokoa Spurs kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Sunderland, timu yake ikitumbukizwa zaidi katika eneo la kushushwa daraja.

Raia huyo wa Italia alimrithi Igor Tudor aliyeongoza Spurs kwa siku 44 pekee, ila mambo yakawa yale yale baada ya Spurs kuendeleza msururu wa mechi 14 bila ushindi, wakisalia bila ushindi mwaka huu wa 2026.

Bao la pekee la mchezo lilipachikwa wavuni na Nordi Mukiele na kuongeza masaibu ya Spurs, ambao pia walimpoteza nahodha wao Cristian Romero kupitia jeraha.

Kwa sasa wamezama katika nafasi ya 18, wakiwa na pointi 30, 2 nyuma ya West Ham United waliopanda juu kutokana na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wolves Ijumaa usiku.

Leo ni zamu ya Manchester United, ambao mara ya mwisho kuingia uwanjani ni siku 25 zilizopita walipoandikisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bournemouth.

Wataialika Leeds United saa nne usiku, fursa yao ya kumaliza katika nafasi ya tatu ikiimarishwa na sare ya Aston Villa hapo jana.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

MGOMO: MATIBABU YALEMAZWA KNH

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *