WAANDALIZI KUIONEA CHAN KWENYE RUNINGA
Waandalizi wote 3 wa mashindano ya ubingwa wa mataifa barani Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani CHAN ambao ni Kenya, Uganda na majirani Tanzania watatazama semi fainali na fainali za mashindano hayo kama mashabiki wa kawaida, baada ya kubanduliwa wikendi iliyopita.
Masaibu yalianzia hapa nchini wakati Madagascar waliwazaba wakenya mabao 4:3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1:1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada, kabla ya Tanzania kufuata mtindo baada ya kuitikia kibano cha 1:0 kwa sifuri mikononi mwa mabingwa mara 2 Morocco.
Uganda waliokuwa wamesalia kama tumaini, walikubali kusimama na ndugu zao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kukubali kupoteza bao 1:0 dhidi ya bingwa mtetezi Senegal siku ya Jumamosi.
Semi fainali hizo zimeratibiwa kusakatwa hapo kesho ambapo Madagascar watatifua kivumbi dhidi ya mwakilishi wa pekee wa shirikisho la CECAFA Sudan katika uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania majira ya saa kumi na moja unusu kabla ya Simba wa Taranga ama Les loi de Taranga wa Senegal kunguruma dhidi ya Morocco katika uwanja wa Nelson Mandela nchini Uganda saa mbili usiku.
Sudan wametinga nusu fainali za mashindano hayo baada ya kuwalaza Algeria mabao 4:2 kupitia mikwaqju ya penalti kufuatia sare ya bao 1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































