KENYA INAUNGA MKONO AFCON 2027 IAHIRISHWE- LOC
Mmojawapo wa wenyeji wa dimba la mataifa bingwa barani Afrika AFCON 2027, Kenya, inaunga mkono kuahirishwa kwa dimba la mwaka ujao hasa kuhusiana na vurugu zinazohusiana na uchaguzi ambazo huenda zikatokea wakati wa mechi hizo.
Hii ni kauli ya mwenyekiti wa kamati andalizi ya mechi hizo humu nchini Nicholas Musonye, akiliambia shirika la habari ya kimataifa ya AFP, muda mfupi baada ya taarifa kuarifu kwamba huenda CAF ikaahirisha dimba hilo hadi mwaka wa 2028 kutokana na ukosefu wa maandalizi ya kutosha kwa wenyeji Kenya, Tanzania na Uganda.
Kikosi cha maafisa wa CAF kinaendeleza ukaguzi wa viwanja na miundomsingi nchini humo kabla ya kikao cha CAF hii leo jijini Dar es Salaam, ambako uwezekano wa kuahirishwa kwa dimba hilo utajadiliwa leo hii.
Rais wa CAF Dakta Patrice Motsepe, awali alisema kuwa ana imani kwamba kipute cha mwaka ujao kitasakatwa jinsi ilivyopangwa.
Hata hivyo, Musonye amesema kuahirishwa kwa ngarambe hiyo kutaifaa Kenya hasa kutokana na joto la kisiasa.
Tayari uwanja wa Kasarani umefungwa ili kupisha ukarabati wa mwisho, huku Nyao ikiratibiwa kufungwa Jumatatu ijayo punde baada ya kukamilika kwa mashindano ya World Rugby SVNS Division II itakayoanza hapo kesho uwanjani humo.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































