#Football #Sports

CARRICK AZUNGUMZIA NAFASI YAKE UNITED

Kocha mkuu wa klabu ya Manchester United Michael Carrick, amesema hana shinikizo katika wadhifa huo licha ya shinikizo tele ambazo watangulizi wake wameshuhudia.

Carrick aliyasema haya baada ya kuiwezesha United kufuzu kombe la klabu bingwa bara Ulaya msimu ujao kufuatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Liverpool hapo jana.

Alipochukua hatamu kutoka kwa Ruben Amorim aliyetimuliwa, lengo kuu la Carrick lilikuwa kuirejesha United katika kombe hilo baada ya kukaa nje kwa misimu mitatu.

Kwa sasa kiungo huyo wa zamani wa United ni miongoni mwa makocha wanaopigiwa debe kupewa wadhifa wa kuinoa United kwa kandarasi ya kudumu, wengine wakiwa kocha wa Bournemouth anayeondoka Andoni Iraola na Mjerumani Julian Nagelsmann.

Katika matokeo mengine, Tottenham iliandikisha ushindi wa pili mfululizo na kujiondoa katika eneo la kushushwa daraja, baada ya wenzao West Ham United kulishwa kichapo.

Tottenham walio chini ya Roberto De Zerbi, waliwashangaza wengi baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Aston Villa.

Leo ni zamu ya Manchester City kupunguza pengo la pointi kati yao na Arsenal, watakapomenyana na Everton katika mechi ya EPL saa nne usiku, huku Chelsea wakichuana na Nottingham Forest saa kumi na moja jioni.

Arsenal ambao wamecheza mechi 2 zaidi ya City, wana pointi 76 kileleni, 6 mbele ya wapinzani wao.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *