#Business

MIKATABA 11 YA KENYA-UFARANSA KUIMARISHA RELI, BANDARI NA UCHUMI DIJITALI  

Rais William Ruto na mwenzake wa ufaransa Emmanuel Macron wameshuhudia kutiwa saini kwa mikataba 11 inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Ufaransa katika uchukuzi, nishati, miundombinu ya kidijitali na biashara.

Mikataba hiyo imetiwa saini katika Ikulu ya Nairobi kufuatia mazungumzo baina ya nchi hizo mbili kabla ya Mkutano wa Africa Forward Summit.Miongoni mwa mikataba muhimu ni ukarabati na uboreshaji wa mradi wa reli ya Nairobi Commuter Rail uliogharimu Sh12.5 bilioni, ambao utaboresha viunganisho vya reli vinavyounganisha Nairobi na miji ikiwa ni pamoja na Syokimau, Embakasi, Ruiru na Kikuyu.

Ruto amesema mradi huo pia utajumuisha laini ya Riruta-Ngong inayojengwa kwa sasa kama sehemu ya juhudi za kuboresha usafiri wa mijini katika eneo la jiji la Nairobi.Kenya na Ufaransa pia zimetia saini makubaliano ya kuanzisha ubia wa ugavi na maendeleo ya miundombinu ya bandari inayokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 104.

Mikataba mingine inahusu mabadiliko ya kidijitali, usalama wa mtandao, akili bandia, huduma za hali ya hewa, uzalishaji endelevu wa mafuta ya anga, ushirikiano wa uchumi wa bluu na upanuzi wa mradi wa Kipeto Wind Power kwa megawati 100 za ziada. Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kukuza mauzo ya chai maalum ya Kenya katika masoko ya Ufaransa na kuimarisha ushirikiano katika huduma za afya, elimu na mafunzo ya kiufundi.

Imetayarishwa na Maurine Amwayi

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *