#Football #Sports

AFC LEOPARDS YASAKA KUJIKWAMUA DHIDI YA NAIBOIS

Miamba wa soka nchini AFC Leopards watashuka uwanjani hii leo dhidi ya Nairobi United, Leopards maarufu kama Ingwe wakilenga kuweka kando masaibu yao na kuonyesha mwamko mpya.

Ingwe wataingia uwanjani leo wakiwa na majeraha ya kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Mathare United wikendi iliyopita, kichapo kilichodidimiza matumaini ya kunyakua taji la ligi kuu ya Kenya, KPL, msimu huu.

Mashabiki wa klabu hiyo wameelekeza macho kwa mwenyekiti Boniface Ambani, aliyeomba msamaha kutokana na kichapo hicho na kuahidi kurekebisha makosa, huku akiiilaumu safu ya ushambulizi kwa kukosa makali.

Ingwe wangali katika nafasi ya 2 wakiwa na alama 43 baada ya kuandikisha ushindi mara 12, wakiwa pointi 10 nyuma ya viongozi Gor Mahia.

Watahitaji si tu kuonyesha kucha zao, bali pia uwezo wa kukwaruza watakapovaana na Naibois, ambao wanalenga ushindi wa pili mfululizo na hivyo kufikisha mechi 5 bila kupoteza.

Naibois ambao wamesakata mechi 21 kutokana na kushiriki kwao kwa mashindano ya CAF, wana pointi 33 katika nafasi ya 9, na wataingia uwanjani wakichochewa na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sofapaka.

Nao Ingwe, ambao ni mabingwa mara 12, huenda wakawa na wakati mgumu kutokana na majeraha kwa wachezaji wake tegemeo Kayci Odhiambo, Emmanuel Lwangu, Maxwell Otieno na Elias Mugune kutokana na majeraha.

Timu hizo 2 zinakutana kwa mara ya pili katika historia yao kwenye mechi za ligi kuu.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *