SHUJAA WAIMARISHA JUHUDI ZA KUPANDISHWA DARAJA HSBC
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji 7 kila upande, Shujaa, imefunga mkondo wa pili wa mashindano ya HSBC SVNS divisheni ya pili kwa ushindi, baada ya kuwatandika wenyeji Uruguay 22-14 usiku wa manane.
Kwa jumla, Shujaa wameandikisha ushindi mara 3 na kupoteza mechi 2, ushindi mwingine ukijiri dhidi ya Canada na Ubelgiji.
Baada ya kuanza kwa kichapo dhidi ya Marekani, Shujaa waliimarisha kampeni yao, na kupata ushindi kabla ya kichapo dhidi ya Ujerumani.
Mkondo wa 3 na wa mwisho utachezwa wikendi ijayo jijini Sao Paulo nchini Brazil ambako timu 4 za kwanza zitapata fursa ya kusakata mwondoano.
Kwa sasa, Shujaa wanashikilia nafasi ya 2 kwa pointi 38, sawa na Marekani walio katika nafasi ya kwanza.
Kwa upande mwingine, kikosi cha akina dada, Kenya Lionesses, kimekuwa na kipindi kigumu, kikiandikisha ushindi mmoja pekee dhidi ya Argentina na kupoteza dhidi ya Uchina, Uhispania na Afrika Kusini.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 



























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































