#Football #Sports

FIFA WORLD CUP: ITALIA WAKARIBIA KUKATA KIU

Timu ya taifa ya kandanda ya Italia itachuana na Bosnia and Herzegovina kwenye fainali za mwondoano wa bara Ulaya kusaka tiketi ya kusakata dimba la kombe la dunia mwaka huu, baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Northern Ireland kwenye semi fainali za mchujo huo.

Wakati uo huo, Wales na Jamhuri ya Ireland zilirambishwa kichapo kichungu kupitia matuta ya penalti kwenye semi fainali nyingine.

Kiungo wa Newcastle Sandro Tonali na Moise Keane, waliifungua Azzurri mabao katika kipindi cha pili, na kuweka hai matumaini ya mabingwa hao mara 4 wa kombe la dunia kushiriki tena dimba hilo baada ya kukosa mara 2 mfululizo.

Kwa sasa Italia watavaana na Bosnia Jumanne wiki ijayo jijini Zenica.

Bosnia walitinga awamu hiyo kufuatia ushindi wa mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Wales.

Mchezaji wa zamani wa Manchester City Edin Dzeko alijitwika Bosnia kichwani na kuwaingiza kwenye fainali hizo, baada ya kufunga bao la kichwa katika dakika za mwisho, akifuta bao la Dan James wa Wales na kulazimisha matuta hayo.

Kwengineko, mchezaji wa Arsenal Viktor Gyokeres alifunga hattrick na kuipa Sweden ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ukraine.

Baada ya mchezo mbovu katika awamu ya makundi, Sweden watamenyana na Poland katika fainali ili kusaka tiketi hiyo.

Robert Lowandowski aliwasaidia Poland kutoka nyuma na kuandikisha ushindi wa mabao 2-1 dhidi la Albania

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *