WELTEJI APIGWA MARUFUKU YA MIAKA 2
Mwanariadha wa mbio za masafa ya kati Diribe Welteji amepigwa marufuku ya kushiriki mbio kwa miaka 2 na mahakama ya kushughulikia masuala ya spoti, CAS, baada ya kukosa kuwasilisha sampuli zake kwa uchunguzi kuhusiana na matumizi ya dawa za kutitimua misuli Februari mwaka jana.
Mahakama hiyo pia ilifutilia mbali matokeo yote ya raia huyo wa Ethiopia katika kipindi hicho, kinachohusisha ushindi wake wa nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 katika mashindano ya World Indoor Championships Nanjing, Uchina mwezi Machi mwaka jana.
Mwanariadha huyo alikuwa amepigwa marufuku ya muda Septemba mwaka jana, na hivyo kukosa kwake kushiriki mbio za ubingwa wa dunia jijini Tokyo, Japan.
Shirikisho la kukabili utumizi wa dawa hizo nchini Ethiopia, ETH-NADO, awali halikumpata na hatia ya kutumia dawa hizo, ila shirikisho la raidha ulimwenguni, likakata rufaa kwa mahakama hiyo likitaka apigwe marufuku ya miaka 4.
Hata hivyo kwenye uamuzi wake, mahakama hiyo ilitoa marufuku ya miaka 2.
Welteji atakuwa na umri wa miaka 25 atakapokamilisha marufuku dhidi yake, huku Makala ya ubingwa wa dunia ya 2027 yakiratibiwa kuanza Septemba 11 jijini Beijing.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 
























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































