BODO GLIMT WAIBANDUA INTER MILAN, ATLETICO NDANI
Klabu ya Bodo Glimt kutoka Norway iliendeleza kisa chake cha kuangusha miamba wa soka bara Ulaya, baada ya kuwapa Inter Milan kichapo cha jumla ya mabao 5-2 nyumbani na ugenini kufuzu raundi ya 16 ya klabu bingwa bara Ulaya.
Glimt ambao wameicharaza Manchester City na Atletico Madrid msimu huu, walifika San Siro jana usiku wakiwa na uongozi wa mabao 3-1 kutokana na ushindi kwenye mkondo wa kwanza nyumbani, na kuanzia walikoachia, wakiandikisha ushindi wa mabao 2-1
Jens Petter Hauge aliyekuwa na miaka miwili migumu San Siro akiwa na AC Milan kabla ya kuondoka, aliwatesa mabeki wa Inter, baadaye akifunga bao katika dakika ya 58 kabla ya kutoa asisti kwa bao lake Hakon Evjen kunako dakika ya 72.
Inter, jinsi ilivyotarajiwa, walirusha kila aina ya kombora langoni pa Glimt kwa juhudi za kubatilisha matokeo, ila wageni wakakaa ngumu na kuyazima, kipa Nikita Haikini akipangua kila kombora lililolenga goli.
Miamba hao wa Italia ambao ni mabingwa mara 3 wa dimba hilo na wakiwa mbele pointi 10 katika jedwali la Serie A, walitarajiwa kuwa na mteremko katika mtanange huo, ila matumaini yao ya kufika angalau fainali walikofika msimu jana, yalizimwa na chipukizi hao wa Norway.
Glimt sasa wanajiandaa kumenyana na City au Sporting CP katika Raundi ya 16 kwenye droo itakayofanyika Ijumaa hii.
Kwenye matokeo mengine, hatrik yake Alexander Sorloth na bao lake Johnny Cardoso yaliwapa Atletico Madrid ushindi wa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya Club Brugge, na jumla ya mabao 7-4 kutoka mikondo miwili, Atletico wakifuzu raundi ya 16.
Newcastle United walifuzu raundi hiyo kwa jumla ya mabao 9-3 dhidi ya Qarabag FK baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 3-2 jana usiku.
Na licha ya sare ya kutofungana, Bayer Leverkusen walifuzu kutokana na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Olympiacos katika mkondo wa kwanza.
Mechi za mkondo wa mwisho zitachezwa leo usiku.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 



























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































