CHEROTICH ALENGA KUREJEA KWENYE USHINDI ZURICH
Bingwa wa dunia wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi Faith Cherotich analenga kurejea kwenye njia ya ushindi katika Riadha za Diamond League jijini Zurich Alhamisi, baada ya kumaliza wa pili katika mashindano ya Lausanne nyuma ya bingwa wa Olimpiki Winfred Yavi wa Bahrain.
Cherotich alikamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 9:01.90, huku Yavi akitwaa ushindi kwa rekodi mpya ya mashindano ya dakika 9:00.04, na Marwa Bouzayani wa Tunisia akimaliza wa tatu kwa dakika 9:05.55.
Mkutano wa Zurich ni wa pili kutoka mwisho katika mzunguko wa Diamond League wa 2026, huku Cherotich akilenga kupata pointi muhimu za kufuzu kwa Fainali za Brussels za Septemba 4 na 5, baada ya kusema ameridhishwa na kiwango alichoonyesha Lausanne na sasa yuko tayari kwa changamoto inayofuata.
Imetayarishwa na Cyrus Sifuna
English 


































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































