NSSF YAKADIRIA FAIDA KUTOKA UJENZI WA RIRONI-MAU SUMMIT
Hazina ya kitaifa kuhusu uhifadhi wa jamii, NSSF, inatarajia kupata faida ya asilimia 18 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 28 ijayo kupitia uwekezaji wake katika mradi wa barabara ya Rironi–Mau Summit.
Barabara hiyo ni sehemu muhimu ya ukanda wa kaskazini maarufu kama Northern Corridor, unaotajwa kuwa mhimili wa mageuzi katika biashara na usafirishaji wa kikanda.
Ushiriki wa NSSF katika makubaliano ya sekta ya umma na binafsi, PPP, na kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya moja kwa moja ya miundombinu iliyowahi kufanywa na hazina ya pensheni nchini.
Mradi wa barabara hiyo unajengwa na kuendeshwa kwa mfumo wa kutoza ushuru watumiaji, ulioundwa kuwezesha wawekezaji kurejesha gharama za ujenzi na kupata faida za uendeshaji kupitia ada za watumiaji kwa kipindi cha miaka 28 hadi 30.
Akizungumza wakati wa kikao na vyombo vya habari jijini Nairobi, Meneja mdhamini wa hazina hiyo David Koros, amesema inatarajia kupata faida ya asilimia 13–15 kwa dola za Kimarekani, ambayo inatafsiriwa kuwa asilimia 18 kwa thamani ya fedha za ndani, kwa umiliki wa hisa wa asilimia 25 katika awamu ya kwanza ya mradi wa barabara, unaokadiriwa kugharimu dola milioni 743 (sawa na Shilingi bilioni 95.8).
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































