MIAMBA WA AFRIKA KUMENYANA ROBO FAINALI CAF CL
Bingwa wa kihistoria mara 12 wa taji la klabu bingwa barani Afrika CAF Champions League, Al Ahly wa Misri, watakabiliana na Esperance Sportive de Tunis wa Tunisisa katika pambano la wazito wa Kaskazini mwa Afrika kwenye awamu ya robo fainali ya ubingwa huo.
Hii ni kulingana na droo iliyofanywa hapo jana nchini Misri, ambapo Al Ahly watasafiri kuelekea Tunisia kwenye mkondo wa kwanza kabla ya kurejea nyumbani kwa marudiano.
Mabingwa watetezi Pyramids FC wa Misri, pia watakuwa safarini kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya AS FAR ya Morocco.
Mamelodi Sundowns wa Afrika Kusini waliomaliza wa pili msimu jana, watakuwa nyumbani dhidi ya mgeni Stade Malien kutoka Mali kwenye mkondo wa kwanza, nao mabingwa wa CAF Confederations Cup msimu jana RS Berkane wa Morocco wakabiliane na Al Hilal wa Sudan.
Mkondo wa kwanza wa mechi hizo utachezwa wikendi ya tarehe 13-15, na marudiano wikendi ya tarehe 20-22 mwezi ujao, huku semi fainali zikisakatawa katika kipindi sawa mwezi Aprili.
Tayari ramani ya semi fainali na fainali imetolewa, na tutaichambua kwa undani katika Kurunzi zijazo na pia katika Mikiki Extra Jumamosi hii.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































