ANTHONY GORDON AVUNJA REKODI YA SHEARER NEWCASTLE
Mshambulizi wa Newcastle United Anthony Gordon, alifunga mabao 4 jana usiku katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ta Qarabag ugenini nchini Azerbaijan, ukiwa ni ushindi mkubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo ya Uingereza.
Mabao hayo pia yalifikisha jumla ya mabao 10 kwa Mwingereza huyo, aliyevunja rekodi ya Allan Shearer na kuwa mchezaji ambaye ameifungia Newcastle mabao mengi zaidi katika dimba la klabu bingwa bara Ulaya.
Kocha mkuu wa Newcastle Eddie Howe, akizungumza kabla ya mechi ya jana, alisema kuwa kikosi chake kililenga kufanya kugeuza dimba hilo kuwa historia, na kufanya kuwa matukio ambayo watu watayazungumzia kwa muda mrefu.
Na hakika, kauli yake ilitimia wakati Gordon alichukua sheria mkononi, kwanza akifunga hattrick kabla ya mkwaju wa penalti, nao Jacob Murphy na Mallick Thiaw wakafunga mengine, huku Elvin Cafarguliyev akiwafuta wenyeji machozi.
Qarabag ni klabu iliyotoka sare ya mabao 2-2 na Chelsea, ikaitandika Benfica, Eintracht Frankfurt na Copenhagen kufika katika mwondoano wa kufuzu Raundi ya 16 ya dimba la klabu bingwa bara Ulaya msimu huu.
Ila jana, Newcastle walikuwa zaidi yao, wakisisitiza pengo lililopo baina ya klabu za ligi kuu ya Uingereza, EPL, na ligi nyingine za Ulaya.
Mkondo wa pili utasakatwa wiki ijayo, na ikiwa Newcastle watafuzu, watajiunga na Manchester City, Liverpool, Chelsea, Totenham na Arsenal katika Raundi ya 16, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu 6 za EPL kutinga awamu hiyo.
Katika matokeo mengine, Bayer Leverkusen walipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Olympiacos nchini Ugiriki, Club Brugge na Atletico Madrid wakagawana hasara ya pointi kutokana na sare ya mabao 3, nao Bodo Glimt wa Norway wakaendeleza rekodi ya kuwaangusha miamba, mara hii mwathiriwa wao akiwa Inter Milan aliyepokezwa kichapo cha mabao 3-1.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































