KANE KIKOSINI DHIDI YA REAL
Mshambulizi wa klabu ya Bayern Munich Harry Kane amejumuishwa kwenye kikosi kilichosafiri nchini Uhispania kwa mtanange wa robo fainali za kombe la klabu bingwa barani Ulaya dhidi ya wenyeji Real Madrid leo usiku.
Kane anayetarajiwa kwa hamu kuongoza mashambulizi katika uwanja wa Santiago Bernebeu, alikuwa mazoezini jana jijini Munich, kabla ya kusafiri na wachezaji wenzake baada ya kuwa na jeraha lililoripotiwa kuwa tatizo dogo lililomweka nje ya mechi za kirafiki za timu yake ya taifa ya Uingereza.
Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 32, pia alikosa mechi dhidi ya Freiburg ambako Bayern walipata ushindi mwembamba wa mabao 3-2.
Kocha mkuu wa Bayern Vincent Kompany, alisema uamuzi wa kumchezesha Kane utafanywa leo.
Bayern na Real watamenyana leo saa nne usiku kwa mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya marudiano wiki ijayo.
Katika mechi nyingine ya mkondo wa kwanza, Arsenal ambao wamepoteza mataji mawili katika mechi mbili mfululizo, watawekwa kwenye ratili watakapovaana na Sporting CP ya Ureno majira ya saa nne usiku.
Wiki 2 zilizopita, Gunners walikuwa wakiwania mataji manne ila udhaifu wao ukajitokeza walipopigwa kwenye mechi ya fainali ya Carabao Cup na Manchester City kabla ya kubanduliwa na Southampton katika robo fainali ya taji la FA.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 


















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































